Rabu, 07 Juni 2023

Watendaji Wa Serikali Zingatieni Sheria - Mhe.Majaliwa *Asema Lengo Ni Kuiepusha Serikali Kuingia Katika Migogoro

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika Maadhimisho ya Miaka Mitano ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwenye Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete jijini Dodoma

Wazirti Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa amewataka watendaji wa idara na taasisi zote za Serikali watekeleze majukumu yao kwa kuzingatia sheria hususan katika huduma wanazozitoa na miradi wanayoisimamia ili kuiepusha Serikali kuingia katika migogoro ambayo inaweza kuepukika.

“Watendaji wote wa Serikali zingatieni sheria, taratibu na kanuni tulizojiwekea kwenye utekelezaji wa majukumu yetu ikiwemo usimamizi wa mikataba na makubaliano mbalimbali tunayoingia ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima inayoweza kutokea ndani ya Serikali na kusababisha kufunguliwa kwa mashauri ya madai na usuluhishi.“

Ameyasema hayo leo (Jumatatu, Juni 5, 2023) katika Maadhimisho ya Miaka Mitano ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali na Uzinduzi wa Mafunzo kwa Mawakili wa Serikali katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma. Amewasisitiza Mawakili hao wawe wabunifu katika kuishauri Serikali ipasavyo kuhusu mashauri yaliyopo.

Waziri Mkuu amesema Mawakili wa Serikali wamepewa dhamana kubwa ya kuitetea Serikali katika uendeshaji wa mashauri ya madai na usuluhishi, hivyo waongeze bidii na juhudi katika utendaji kazi na wafanye kazi kwa uzalendo, weledi na uadilifu.

“Serikali kwa upande wake itaendelea kuitengea bajeti ya kutosha Ofisi hii kwa kadri rasilimali zitakavyoruhusu. Vilevile, itaendelea kuipatia rasilimali kerikil ya kutosha sambamba na kuwezesha upatikanaji wa mafunzo kwenye maeneo ya kimkakati kama vile mafuta na gesi, uwekezaji, sheria za anga na madini.“

Waziri Mkuu amesema ili kuhakikisha kuwa Serikali inaendelea kuimarisha diplomasia ya uchumi na kuendelea kujenga mazingira shindani ya kuvutia wawekezaji, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwa kushirikiana na Wizara, Idara na taasisi za Serikali itatue migogoro kwa njia ya majadiliano na maridhiano.

Mheshimiwa Majaliwa amesema faida ya kutatua migogoro kwa njia ya majadiliano ni pamoja na kupunguza gharama, kuokoa muda na kulinda mahusiano ya kibiashara na kidiplomasia. “Nisisitize kuwa, bado Serikali yetu inahitaji wawakezaji katika kuchangia ukuaji wa haraka wa uchumi na pato la Taifa.“

“Wizara, Idara na Taasisi za Serikali fanyeni kazi kwa karibu Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali katika uendeshaji wa mashauri ya madai na usuluhishi yanayohusu Serikali kwani ndiyo yenye mamlaka ya kisheria ya kusimamia mashauri yanayohusu Serikali na Taasisi zake ndani na nje ya nchi.“

Pia, Waziri Mkuu ametoa msisitizo kwa taasisi zote za umma zenye Mawakili wa Serikali kuzingatia suala la utatuzi wa kero za wananchi ili kupunguza mlundikano wa mashauri ambayo hayana ulazima wa kufikishwa Mahakamani hususan katika kipindi hiki cha miaka mitatu ambacho Wizara ya Katiba na Sheria inatekeleza Kampeni ya Kitaifa ya Msaada wa Kisheria nchini kote “Mama Samia Legal Aid Campaign”

Kwa upande wake, Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro amesema katika kipindi cha miaka mitano tangu kuanzishwa kwa ofisi hiyo ambayo inafanya kazi kwa weledi imeweza kuisaidia Serikali kuokoa zaidi ya shilingi trilioni saba kutokana na kutatua baadhi ya mogogoro kwa njia ya usuluhishi.

Naye, Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Luhende amesema baada ya uzinduzi huo wanatarajia kuendesha mafunzo ya siku tatu kwa Mawakili wa Serikali zaidi ya 600 ili kuwaongezea ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikata utepe kuzindua  Jarida Maalum la Miaka  Mitano ya Ofisi ya Wakili wa Serikali kwenye Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete jijini Dodoma, Juni 5, 2023. Wengine kutoka kushoto ni Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro, Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt  Boniface Luhende na kulia ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Dkt. Eliezer Feleshi.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akionesha  Jarida Maalum la Miaka  Mitano ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali baada ya kulizindua  kwenye Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete jijini Dodoma, Juni 5, 2023. Wengine kutoka kushoto ni Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro, Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt  boniface Luhende na kulia ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Dkt. Eliezer Feleshi. 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea tuzo ya heshima kutoka kwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro ya kutambua mchango wake katika kuanzishwa kwa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kabla ya kuzungumza katika Maadhimisho ya Miaka Mitano ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwenye Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete jijini Dodoma, Juni 5, 2023. Katikati ni Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniface Luhende.

Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan Awaandalia Hafla Ya Kuwapongeza Wachezaji Wa Timu Ya Yanga, Ikulu Jijini Dar Es Salaam

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipokea Medali kama ishara ya shukrani kutoka kwa Rais wa Klabu ya Yanga Eng. Hersi Said wakati wa hafla ya kuipongeza timu ya Yanga iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 05 June, 2023.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na Wachezaji na Makocha wa timu ya Yanga wakati wa hafla ya kuwapongeza kwa kufanikiwa kufika na kucheza mchezo wa Fainali ya Mashindano ya Shirikisho Afrika (CAF) nchini Algeria. Hafla hiyo ya kuwapongeza Yanga imefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 05 June, 2023.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi, wachezaji wa timu ya Yanga pamoja na wadau mbalimbali wa michezo wakati wa hafla aliyowaandalia kuwapongeza Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Wachezaji na Makocha wa Timu ya Yanga wakiwa kwenye hafla ya kupongezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, Ikulu Jijini Dar es Salaam 


Viongozi, wachezaji wa zamani, waandishi wa Habari, batu maarufu, wasanii pamoja na wadau mbalimbali wa michezo wakiwa kwenye hafla ya kuipongeza timu ya Yanga iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam







Makamu Wa Rais Wa Jamhuri Ya Muungano Wa Tanzania Mhe.Dkt. Philip Mpango Akiwasili Mkoani Tabora Kwa Ufunguzi Wa Umisseta

 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Tabora leo tarehe 06 Juni 2023. Makamu wa Rais amewasili Mkoani Tabora kwaajili ya Ufunguzi wa Mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA yanayofanyika katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi.


Milango Kwa Wawekezaji Wa Biashara Ya Kaboni

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo amesema Serikali inaendelea kufungua milango kwa wawekezaji wa Biashara ili kuhifadhi mazingira.

Amesema hayo leo Juni 06, 2023 wakati wa kikao na Mkuu wa Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora Dkt. Rashid Chuachua pamoja na ujumbe wake waliomtembelea kwa Kuwasilisha taarifa ya kusudio la kuanzisha mradi wa hifadhi ya misitu kwa ajili ya biashara ya kaboni.

Ameupongeza uongozi wa wilaya hiyo kwa kuhifadhi misitu na nia yao ya kuwekeza katika biashara ya Kaboni akisema kuwa mbali ya kuhifadhi mazingira lakini pia itawa chanzo cha mapato ya halmashauri.

“Kutokana na Mikataba ya Kimataifa ya Mabadilkiko ya Tabianchi, segi kama nchi tumejipanga vizuri kuhakikisha wananchi wanafaidika na biashara hii na ndio maana tumeandaa kanuni na mwongozo,” amesema.

Pia, amesema Ofisi ya Makamu wa Rais ipo tayari kuendelea kutoa elimu kwa umma ili kuwapa uelewa wananchi kutoka maeneo mbalimbali nchini zikiwemo halmashauri kuhusu faida za kupanda miti na kuhifadhi misitu.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kaliua Dkt. Chuachua amesema kusudio la kuanzisha mradi wa hifadhi ya misitu kwsa ajili ya hewa ya ukaa ni kupata fursa ya biashara hiyo ambayo faida yake itasaidia kuboresha huduma kwa wananchi wake.

Amesema wilaya ina fursa kubwa ya kuwekeza katika biashara hiyo kwa kuzingato kuwa kilomita za mraba 12,084.5 sawa na asilimia 86 ya eneo lote la wilaya hiyo.

Hivyo amesema kuwa mradi huo ni muhimu kwan utasaidia kuongeza wigo wa mapato ya halmashauri ambayo kwa asilimi 80 yaekuwa yakitona na mazao ya kilimo.

Dkt. Chuachua ameongeza kwa kusema kuwa mradi utasaidia katika kutunza mazingira ya ardhi oevu ambayo ndio chanzo cha maji katika Mto Malagarasi na Ziwa Tanganyika.  

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Andrew Komba amesema kuwa Biashara ya Kimataifa inasimamiwa na Umoja wa Mataifa kwa lengo kuwezesha nchi wanachama kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Dkt. Komba amesema kuwa mabadiliko ya tabianchi yanasababisha ongezeko la joto duniani na vipndi vya baridi na mvua kupungua hali inayochangia ukame.

Hivyo amesema misitu ikiwa mingi itasaidia katika kunyonya gesijoto inayochangiwa na shughuli za kibinadamu zikiwemo moshi unaotokana na magari na viwanda.

Serikali Ya Mapinduzi Ya Zanzibar Inaridhishwa Na Kazi Kubwa Inayofanywa Na Timu Nzima Ya Unicef

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiwa katika mazungumza na  mgeni wake Mwakilishi Mkaazi wa UNICEF  Nchini Tanzania Bi. Shalina Baguhuna, alipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.06/06/2023.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na  mgeni wake Mwakilishi Mkaazi wa UNICEF  Nchini Tanzania Bi. Shalina Baguhuna (kulia kwa Rais) alipofika Ikulu Jijini Zanzibar leo 6-6-2-023 katika ukumbi wa Ikulu Zanzibar na  (kushoto kwa Rais) Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said, mazungumzo hayo yliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akikabidhi zawadi ya Mlango wa Zanzibar kwa  mgeni wake Mwakilishi Mkaazi wa UNICEF  Nchini Tanzania Bi. Shalina Baguhuna, alipofika Ikulu Jijini Zanzibar akiwa na Ujumbe wake leo katika ukumbi wa Ikulu Zanzibar
 

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema inajivunia ushirikiano wake na Wadau wa Maendelo likiwemo Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Elimu na Watoto diniani, (UNICEF).

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi alisema hayo Ikulu, Zanzibar alipozungumza na Mwakilishi Mkazi wa UNICEF, Tanzania Bi. Shalini Bahuguna aliefika kwaajili ya kumuaga baada ya kumaliza kwa muda wake wa utumishi kwenye shirika hilo.

Dk. Mwinyi alisema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaridhishwa na kazi kubwa inayofanywa na timu nzima ya UNICEF, Tanzania kupitia ushirikiano wake kwani wako bega kwa bega katika kuimarisha masuala yanayohusu ustawi wa watoto nchini.

“UNICEF imefanya makubwa Tanzania hususani ushirikiano wake wa karibu katika kuiungamkono Serikali yetu kwenye masuala mbalimbali ya maendeleo, wamefanya mengi siwezi kuyaonesha maeneo yote sababu ni mengi mno.” alifafanua Rais Dk. Mwinyi.

Pia Dk. Mwinyi, alimpongeza Bi. Shalini kwa jitihada zake, kwa kipindi chote alichofanyakazi na UNICEF hapa nchini akieleza mchango mkubwa walioutoa kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hasa katika miradi ya maendeleo iliyotekelezwa na shirika hilo katika kuiunga mkono SMZ.

Dk. Mwinyi alimweleza Mwakilishi huyo kwamba, daima Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kulishukuru Shirika la UNICEF kwa kuiunga mkono Zanzibar kwenye masuala ya Afya na Elimu.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Bi. Shalini alimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa uongozi wake hasa katika kuzisimamia vema rasilimali za Zanzibar kwenye ujenzi wa maendeleo ya Wazanzibari wa maeneo yote ya Unguja na Pemba.

Alimsifu Dk. Mwinyi kuwa Kiongozi wa mfano hasa kwa kukinawirisha kimaendeleo Kisiwa cha Pemba na mageuzi makubwa aliyofanya kwenye sekta za afya na Elimu Zanzibar.

Vilevile bi Bi. Shalini ameisifu za Zanzibar kwa kufanikiwa kutekeleza malengo ya Mileniam kwani imefanikiwa kwenye suala zima la kudumisha usafiwa mazingira kwa maeneo mengi ya miji.

Akizungumzia mafanikio katika ustawi wa masuala ya watoto, Mwakilishi huyo wa UNICEF aliipongeza Serikali ya Dk. Mwinyi na kueleza kuwa Zanzibar imefanikiwa kwa asilimia 75 kuwarejesha skuli watoto wengi walioacha masomo kwa mazingira tofauti waliyokumbana nayo kwenye makuzi yao.

UNICEF ni Shirika la Umoja wa Mataifa (UN) lililoanzishwa tangu mwaka 1946 New York, Marekani, linashughulika na masuala ya Elimu na Watoto duniani, linafanyakazi kwenye maeneo zaidi ya 190 duniani kote, katika kuwafikia watoto na vijana walio kwenye matatizo kutokana na majanga mbalimbali kwa kuboresha chanjo kwa watoto na kutoa lishe bora katika kuimarisha huduma za dharura mbali na mambo mengine yanayowahusu watoto.

IDARA YA MAWASILINO, IKULU ZANZIBAR.

Makamu Wa Pili Wa Rais Wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Amezindua Kampeni Ya Msaada Wa Kisheria

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akizungumza na Wadau mbali mbali wa Sheria pamoja na Wasaidizi wa Sheria wakati akizindua Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia kwa Mkoa wa Mjini Magharibi uliofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil kikwajuni Jijini Zanzibar.
Baadhi ya Viongozi, Wadau wa Sheria na Wasaidizi wa Sheria wakimsikiliza kwa makini Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akihutubia wakati akizindua Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia kwa Mkoa wa Mjini Magharibi uliofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni Jijini Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema kampeni ya huduma ya Msaada wa kisheria ya Mama Samia inalenga kulinda na kukuza upatikanaji wa haki kupitia huduma za msaada wa kisheria Nchini.                                                                      

Ameyasema hayo wakati akizindua kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia Mkoa wa Mjini Magharibi katika ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni Jijini Zanzibar. 

 

Ameeleza kuwa kampeni hiyo itaimarisha upatikanaji wa haki kwa wananchi wasiojiweza ,wanawake, watoto pamoja na makundi mengine yanayoishi katika mazingira magumu ,kuimarisha amani na utulivu na kuleta utengamano wa Kitaifa.

 

Sambamba na hayo Mhe. Hemed amewaagiza wanaohusika na utekelezaji wa Kampeni hiyo kutekeleza majukumu yao ipasavyo ili kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi za kupiga vita na kukemea vitendo vya ukatili wa kijinsia, udhalilishaji na migogoro ya ardhi vitendo ambavyo vimekua vikijitokeza katika jamii.

 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewaagiza viongozi wa Serikali ya Mkoa wakiwemo Madiwani na Masheha kuwa mabalozi wazuri katika kupiga vita vitendo vya kikatili kwa kusimamia haki na sheria katika kufanya maamuzi. 

 

Aidha Mhe. Hemed amewapongeza wasaidizi wa kisheria Nchini kwa kuendelea kuwasaidia wananchi wasiojiweza ili kupata haki zao kwa mujibu wa sheria.

 

Aidha amewapongeza wadau mbali mbali wakiwemo Jeshi la Polisi, Mahkama, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu na Ofisi ya Mkurugenzi wa mashtaka kwa kuhakikisha kila mwananchi anapata haki yake kwa mujibu wa Sheria juhudi ambazo zinaleta taswira njema kwa Wananchi kuwa na imani na wadau hao.

 

Nae waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Mhe. Harun Ali Suleiman amesema Kampeni hiyo itasaidia kupunguza dhulma, unyanyasaji na ukatili wa kijinsia katika jamii.

 

Amesema wananchi wengi wanahitaji msaada wa kisheria ambapo ni wazi kuwa wengi wamenufaika na msaada huo wakiwemo wazee wanaofatilia kiinua Mgongo na Pensheni jamii.

 

Nae Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Mhe. Idriss Kitwana Mustafa amesema Serikali ya Mkoa itakuwa karibu na wananchi katika kuhakikisha kampeni hiyo inafanikiwa ipasavyo kwa lengo la kumuunga Mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi.

 

Kampeni ya Msaada wa kisheria ya Mama Samia imezinduliwa leo kwa lengo la kuwafikia wananchi hasa wasio na uwezo ikiwa na kauli mbiu isemeyo "Msaada wa kisheria kwa haki, usawa, amani na maendeleo "





Kuna Umuhimu Wa Kupewa Mafunzo Kwa Wafanyakazi Ili Waweze Kufanya Kazi Zao Kwa Uweledi

Na Maulid Yussuf  - WMJJWW 

Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Bi.Abeida Rashid Abdallah amesema kuna umuhimu wa kupewa mafunzo kwa wafanyakazi ili waweze kufanya kazi zao kwa weledi.

Akifungua mafunzo kwa wakuu wa vitengo na divisheni wa Wizara hiyo katika ukumbi wa Sebleni kwa Wazee, Bi Abeida amesema ni lazima kuwakumbusha wafanyakazi, sheria, miongozo pamoja na sera za utumishi wa umma ili kuleta ufanisi katika kazi.

Aidha amewataka wakuu hao kufahamu haki na wajibu ni vitu vinavyoenda sambamba, hivyo ni vyema kuhakikisha wanawakumbusha watendaji wao juu ya wajibu wao wa kazi ili nao wapate haki zao ipasavyo.

Aidha amewataka kuhakikisha wanawashirikisha watendaji wao wa chini katika masuala mbalimbali ya kazi ili nao waweze kujenga uelewa katika masuala mbalimbali ya ofisi yao.

Mapema Mkurugenzi Uendeshaji na Utumishi Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Bwana Salum Khamis Rashid amesema kufanyika kwa mafunzo hayo ni muendelezo wa kuwajengea uzoefu wafanyakazi katika utendaji wao wa kazi.

Amesema katika mafunzo hayo mada mbalimbali zitafundishwa ikiwemo, kujitambua, rushwa, utunzaji wa siri, nidhamu za kazi pamoja na masuala mengine.

Wakiwasilisha mada  wakufunzi kutoka Ofisi ya Rais katiba Sheria, Utumishi na Utawala bora ndugu Yussuf Mohd  Suleiman na Ndugu Mustafa Khamis Simai wamesema ni wajibu wa mtumishi wa umma kuhakikisha anatunza siri za kazi, kutotumia mali za Serikali kwa maslahi yake, pamoja na kuhakikisha anakuwa na nidhamu kazini.

Wakitoa michango yao baadhi ya Wakuu hao wamesema kuna baadhi ya viongozi wao wamekuwa na lugha mbaya wanapozungumza na watendaji wao jambo ambalo linaweza kuleta athari katika utendaji, hivyo wameomba nao wawajibishwe kwa mujibu wa sheria za kiutumishi.

Mafunzo hayo ya siku mbili yameandaliwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto chini ya Idara ya Uendeshaji na Utumishi wa Wizara hiyo.