Rabu, 07 Juni 2023

Kuna Umuhimu Wa Kupewa Mafunzo Kwa Wafanyakazi Ili Waweze Kufanya Kazi Zao Kwa Uweledi

Na Maulid Yussuf  - WMJJWW 

Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Bi.Abeida Rashid Abdallah amesema kuna umuhimu wa kupewa mafunzo kwa wafanyakazi ili waweze kufanya kazi zao kwa weledi.

Akifungua mafunzo kwa wakuu wa vitengo na divisheni wa Wizara hiyo katika ukumbi wa Sebleni kwa Wazee, Bi Abeida amesema ni lazima kuwakumbusha wafanyakazi, sheria, miongozo pamoja na sera za utumishi wa umma ili kuleta ufanisi katika kazi.

Aidha amewataka wakuu hao kufahamu haki na wajibu ni vitu vinavyoenda sambamba, hivyo ni vyema kuhakikisha wanawakumbusha watendaji wao juu ya wajibu wao wa kazi ili nao wapate haki zao ipasavyo.

Aidha amewataka kuhakikisha wanawashirikisha watendaji wao wa chini katika masuala mbalimbali ya kazi ili nao waweze kujenga uelewa katika masuala mbalimbali ya ofisi yao.

Mapema Mkurugenzi Uendeshaji na Utumishi Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Bwana Salum Khamis Rashid amesema kufanyika kwa mafunzo hayo ni muendelezo wa kuwajengea uzoefu wafanyakazi katika utendaji wao wa kazi.

Amesema katika mafunzo hayo mada mbalimbali zitafundishwa ikiwemo, kujitambua, rushwa, utunzaji wa siri, nidhamu za kazi pamoja na masuala mengine.

Wakiwasilisha mada  wakufunzi kutoka Ofisi ya Rais katiba Sheria, Utumishi na Utawala bora ndugu Yussuf Mohd  Suleiman na Ndugu Mustafa Khamis Simai wamesema ni wajibu wa mtumishi wa umma kuhakikisha anatunza siri za kazi, kutotumia mali za Serikali kwa maslahi yake, pamoja na kuhakikisha anakuwa na nidhamu kazini.

Wakitoa michango yao baadhi ya Wakuu hao wamesema kuna baadhi ya viongozi wao wamekuwa na lugha mbaya wanapozungumza na watendaji wao jambo ambalo linaweza kuleta athari katika utendaji, hivyo wameomba nao wawajibishwe kwa mujibu wa sheria za kiutumishi.

Mafunzo hayo ya siku mbili yameandaliwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto chini ya Idara ya Uendeshaji na Utumishi wa Wizara hiyo.

0 komentar:

Posting Komentar